Mkurugenzi Mtendaji Taasisi ya Elimu ya Zanzibar Nd. Abdalla Mohammed Mussa amewataka walimu kuwatayari kuufanyia kazi Mtaala mpya wa Sekondari ambao unakusudia Kuwawezesha wanafunzi kuwa na ujuzi na utambuzi wa fursa zilizomo kwenye jamii. Akifungua mafunzo ya siku nne kwa wakufunzi wa walimu (TOT) huko katika Kituo cha walimu Michakaini kisiwani Pemba amesema katika utekelezaji wa Mtaala huo ni lazima walimu kuwa na utayari kwani wao ndio watekelezaji wakubwa wa mtaala huo wanaotegemewa katika kuwaandaa wanafunzi darasani. Aidha amewataka Wakufunzi wa walimu wanaopatiwa mafunzo hayo kwenda kuwafahamisha walimu kuwa Mabadiliko ya Mtaala ni jambo la kawaida kulingana na mahitaji ya jamii husika pamoja na Mabadiliko ya sayansi na teknolojia. Amesema Mafunzo hayo yatawasaidia walimu katika kuutumia Mtaala mpya wa umahiri kwa Ngazi ya Sekondari. Akiwasilisha Mada ya Utelezaji wa Mtaala Ulioboreshwa kwa ngazi ya Sekondari Muwezeshaji Kutoka Taasisisi ya Elimu Tanzania Hwago Hassan Hwago amesema Elimu ya Sekondari sasa itakua na mikondo miwili ambayo ni mikondo wa Jumla na Mkondo wa Amali. Ameeleza kuwa Mtaala mpya wa Sekondari umetoa fursa kwa wanafunzi kujifunza Elimu ya Amali ili kuwawezesha wanafunzi hao kujiajiri wanapomaliza masomo yao.
Taasisi ya Elimu ya Zanzibar ni Wakala wa Serikali chini ya Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali Zanzibar iliyoanzishwa mwaka 2011 kwa kuzingatia matakwa ya Sera ya Elimu ya mwaka 2006. Serikali ya Mapinduzi Zanzibar imeona kuna umuhimu wa kuwa na chombo cha kuratibu na kusimamia mitaala na utafiti wa elimu ili kuimarisha ubora wa elimu hapa Zanzibar. Kwa mujibu wa Sheria Namba 4 ya mwaka 2016 iliyoanzisha Taasisi ya Elimu ya Zanzibar, Taasisi ina mamlaka ya kutayarisha mitaala, vifaa vya kufundishia na kujifunzia kwa skuli za Maandalizi, Msingi, Sekondari, Vyuo vya Ualimu na Elimu isiyorasmi na Watu wazima. Aidha Taasisi inajukumu la kufanya tafiti za kielimu na kutoa mafunzo juu ya utekelezaji wa mitaala.
Kiongozi wa kuandaa mitaala bora na sahihi kutokana na utafiti kwa matumizi ya skuli na vyuo vya ualimu Zanzibar.
Kuongoza utaratibu wa kuandaa mitaala na vifaa bora vya kufundishia na kujifunzia kwa lengo la kuwa na elimu bora na sahihi kupitia utafifiti na ushirikishwaji wa wadau ili kukidhi matakwa ya watu wa Zanzibar
Huduma zinazotolewa na Taasisi ya Elimu ya Zanzibar.
Kuishauri Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar juu ya mambo yanayohusiana na ukuzaji Mitaala ya Elimu ya Maandalizi, Msingi, Elimu ya Sekondari pamoja na Vyuo vya Ualimu
Kufanya tafiti za Elimu na Kuthibiti Ubora kwenye vifaa vya kufundishia na kujifunzia
Kuratibu Utayarishaji wa Vifaa vya Kufundishia na Kujifunzia kwa walimu na wanafunzi
Kutoa Mafunzo kazini yanayohusiana na Mitaala na Vifaa vya Kufundishia na Kujifunzia