Tarehe Iliyotumwa 2023-02-26 15:44:41
Mafunzo ya Upitiaji wa vitabu katika mtaala mpya
Mkurugenzi Mtendaji Taasisi ya Elimu ya Zanzibar mwalim Abdalla Mohammed Mussa amewataka wadau watakaoshiriki katika kazi ya upitiaji wa vitabu vipya vya maandalizi na msingi kuwa makini katika kazi hiyo ili kuepusha makosa madogo madogo yatakayosababisha kurejesha nyuma juhudi za Serikali.
Mwalim Abdalla ametoa wito huo alipokuwa akifungua mafunzo ya siku tatu ya kutathmini miswada ya vitabu vya kiada na viongozi vya mwalim kwa wadau hao yanayofanyika katika skuli ya Dk Shein Rahaleo.
Amesema lengo la kutolewa mafunzo hayo ni kuhakikisha vitabu vitakapoanza kutumika vinakuwa na ubora zaidi na kuepusha makosa kulingana na walengwa husika na mazingira halisi ya Zanzibar.
Mkurugenzi Abdalla katika hafla hiyo alitumia fursa ya kuwapongeza wadau mbalimbali ambao walishiriki katika uandaaji wa vitabu hivyo kuanzia mwanzo hadi hatua iliyofikia.
Kwa upande wake Meneja Idara ya Utafiti na Udhibit Ubora kutoka Taasisi ya Elimu ya Zanzibar Nd Faridu Muhammed Wakil amesema mafunzo hayo yatasaidia kwa kiasi kikubwa kuhakisha vitabu hivyo vinakuwa Bora zaidi kwa watumiaji .
Mkufunzi wa mafunzo hayo ambae ni mhariri kutoka shirika la Oxford Frederik Silvester amesema katika kuvipitia vitabu hivyo washiriki hao watambue kuwa vitabu hivyo vinakwenda kuwaandaa wataalamu wa baadae.
Miswada ambayo inatarajiwa kupitiwa baada ya mafunzo hayo ni mswada wa vitabu vya darasa la maandalizi mwaka wa kwanza darasa la kwanza, la nne na la saba
Mafunzo hayo yameandaliwa na Taasisi ya Elimu ya Zanzibar kupitia Idara ya Utafiti na Udhibiti ubora.