Muendelezo wa Utoaji wa Mafunzo kwa Walimu - Pemba
Taasisi ya Elimu Zanzibar imesema itaendelea kutoa mafunzo ya mara kwa mara kwa Walimu wa maandalizi na msingi juu ya mtaala mpya wa umahiri ili kuwajengea uwezo Walimu katika ufundishaji wao. Akifunga mafunzo ya siku 5 ya Mtaala wa umahiri kwa walimu wa maandalizi mwaka wa pili wa Mkoa wa Kusini Pemba huko kituo cha Walimu Michakaini Kisiwani Pemba, Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Elimu ya Zanzibar Abdalla Mohamed Mussa amesema kufuatia mabadiliko ya mtaala Taasisi ya Elimu inalazimika kutoa Mafunzo kwa walimu na kuwapatia vifaa vya kufundishia ikiwemo vitabu. Amesema serikali kupitia Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali Zanzibar inaendelea kufanya mageuzi makubwa katika sekta ya Elimu, hivyo ni vyema walimu wakaendana na mageuzi hayo ili waweze kutekeleza kazi zao kwa weledi na kutengeneza Taifa lenye wasomi. Mapema Mratibu wa Taasisi ya Elimu Zanzibar Kisiwani Pemba Bi Asha Soud Nassor amesema walimu wameonyesha maendeleo mazuri katika muda wa mafunzo hayo ya siku tano hivyo jamii itegemee mabadiliko makubwa kwa wanafunzi wa skuli za Serikali na binafsi. Wakizungumzia mafunzo hayo baadhi ya waalimu wameipongeza Taasisi ya Elimu ya Zanzibar kwa kusimamia vyema Mafunzo hayo na kuahidi kuwa mabalozi wazuri kwa walimu wengine Zaidi ya walimu Elfu Sita wanaendelea kupatiwa Mafunzo hayo wakiwemo wa skuli za Serikali na za Binafsi kwa wilaya zote za Unguja na Pemba.